Header Ads

TUPIGANIE KUTAMBULIKA KWA UTU WA MWANAMKE

Na Happiness Katabazi

HOJA ya Jinsia inaweza kupoteza maana yake ikiwa wanawake tutakubali kwamba usawa wa jinsia maana yake ni kugawana madaraka, kazi, majukumu ya ndani ya nyumba, hata mavazi sawa na wanaume. Hii siyo sawa.

Suala la jinsia lazima lizingatie upekee katika jinsia kwa maana kamili kwamba mwanamke ana upekee wake na kwamba upekee huo ni muhimu kwa uwepo wa binadamu. Na upekee huo usilinganishwe na uanaume.

Hii ina maana kwamba mwanamke ni kamili bila kulinganishwa na mwanaume na wala upekee wa mwanaume hauna uhusiano na ubora wa jinsia ya kike.

Huo ndio mtazamo wangu wa hoja ya jinsia na ukumbozi wa mwanamke.

Takwimu zinaonyesha kwamba wanawake wengi sasa wameshika nafasi za uongozi na wameweza kufanya kazi za kitaaluma sawa na wanaume. Hili ni jambo la kuridhisha sana.Wanawake sasa wamejikomboa, wamejithamini na kuwa bora zaidi.

Kama asilimia 30 ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wanawake, haitudhibitishii uwezo wa wanawake kwenye medani ya siasa na uongozi wa kitaifa.

Takwimu hizo hazimaanishi kwamba wanaume sasa wako tayari kuongozwa na wanawake na wala haimaanishi wanawake wenyewe wako tayari kuongozwa na wanawake wenzao.

Viti maalum vinaweza kuwa chimbuko la ukombozi kama vile vinavyoweza kugeuka kuwa chimbuko la ulemavu wa kisiasa kwa wanawake.

Mwanafalsafa wa kale wa Ugiriki , Aristotle, aliyezaliwa mwaka 384 Kabla ya Kristo, alichangia kiasi kikubwa kubadilisha fikra na mtazamo wa maisha barani Ulaya.

Aristotle aliwahi kusema, “Tofauti kati ya mtu wa kawaida na shujaa ni kwamba mtu shujaa huchukulia kila kitu kama changamoto ; wakati mtu wa kawaida huchukulia kila kitu kuwa ni baraka ama laana.”

Kwa hiyo leo tunaposherehekea siku ya wanawake duniani, sisi wanawake tujiulize utu wa mwanamke ni kitu gani tofauti na utu wa mwanaume?

Vinginevyo mashindano ya kijinsia siyo tu yanaweza kuvunja familia, bali pia yanaweza kumletea mwanamke balaa kubwa. Tukumbuke kila mara familia inapovunjika, muathirika mkuu ni mwanamke.

Kila mara mwanamke anapotakiwa kutenda jukumu la kijamii, huathirika kwa kuwa ubora wa kazi zake utatathminiwa kwa vigezo vya wanaume.

Sifa kwa mwanamke ni kuwa kama mwanaume na si vinginevyo. Je, wanawake wenzangu hilo ndilo tunaloadhimisha leo?

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumapili, Machi 8 mwaka 2009

1 comment:

nyahbingi worrior. said...

samahani fungua kurasa ya kuchangia mawazo kuhusu jumuiya ya wanablogu tanzania.

http://blogutanzania.blogspot.com/

www.ringojr.wordpress.com

Powered by Blogger.