Header Ads

GHAFLA VIONGOZI WA CCM WANAWAANGUKIA WANANCHI

Na Happiness Katabazi

GHAFLA Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) wanawaangukia wananchi kumbe msimu wa kura umewadia.

Mwaka 2005, CCM ilinadi wagombea wake kwa kuwaaidi wananchi maisha bora kwa kila Mtanzania.Msemo huo ulichapishwa kila gazeti, ulitangazwa kila redio,Televisheni,fulana, kanga na vipeperushi mbalimnali kwa wingi kwa wapiga kura.

Ukiacha thamani ya vipepelushi yenyewe ambayo ilighalimu mamilioni ya fedha , viongozi wa chama hicho waliomba kura kwa kila njia, mbinu ikiwa ni pamoja na kutoa takrima ambayo mwaka 2006 Mahakama Kuu,iliitangaza kuwa ni rushwa , fedha, chakula, vinywaji nk.

Kwa hakika msemo wa kasi mpya ari mpya na nguvu mpya uliambatana na nguvu hizo za fedha ambazo leo tumejua ni hizi za EPA na mikataba ya manunuzi ya umma na madini.

Tunao uhakika sasa kwamba wapiga kura wengi wa nchi hii walidanganywa kwa usanii huo mkubwa.Leo hakuna kiongozi wa kuachaguliwa awamu ya nne anayeweza kukwepa tuhuma za kuwa alichaguliwa kwa kutumia mbinu hizi chafu.

Hakuna aliyeyaona maisha bora hayo miaka mitatu sasa baada ya uchaguzi ule wa mwaka 2005, wala hakuna matumani kwamba maisha hayo bora kwa kila mtanzania yatapatikana katika kipindi cha miaka miwili iliyosalia.

Kwa mara ya kwanza katika histoaria ya nchi yetu serikali iliyoingia madarakani kwa mara ya kwanza ili kumba na mfululizo wa kashfa za wizi wa mali za umma, rushwa na ubadhilifu hata ikibidi serikali ya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kujiudhuru.

Tatizo ni kwamba serikali hiyo iliyojiudhuri kwa tuhuma za rushwa na shetani hilo la rushwa limo ndani ya serikali hiyo hadi sasa.Serikali iliyochaguliwa kwa rushwa kamwe aisafishiki.

Leo ilibidi wananchi waikabe koo serikali hiyo iteme donge la Dowans.Wananchi wasingesimama kidete siku chache zilizopita, donge hilo lingeishamezwa na serikali yetu.

Kipindi kilichopo tunashuhudia mawaziri , wabunge na madiwani wakimimika kwenye majimbo yao ya uchaguzi.Mawaziri wakitumia nyenzo za kiserikali za magari na misaada kupelekea wapiga kura katika majimbo yao.

Ghafla tumeshuhudia lugha nyenyekevu kutoka kwa viongozi na kwa mara ya kwanza tumeanza kuwasikia wabunge wakitetea wananchi wao wanaodhurumiwa haki zao kupitia sera mbalimbali za serikali.

Kuanzia kwa Rais Jakaya Kikwete, tumeanza kusikia utetezi kwa wananchi wanaobomolewa makazi na kunyang’anywa ardhi zao ili kuwapisha wawekezaji na miradi mbalimbali ya maendeleo bila malipo ya fidia.

Hiki ni kilio cha wananchi kila mahali nchini.Serikali yetu haijali maslahi yao bala inajali maslahi ya wawekezaji na maslahi ya miradi .

Umaskini wa raia binafsi unasababishwa na serikali yenyewe kwa kuwa kila mara wapolazimika kuama makazi na ardhi mbadala na wala fidia haitoshi kujenga makazi mapya.

Tungetegema kama wananchi wangelitambua hilo na kusimama kidete kushika fimbo kumchapa kila kiongozi wa CCM anayejaribu kuwoamba kura.Ni usanii mtupu.

Kwa upande mwingine tumeona sasa baadhi ya viongozi wanaotoka maeneo ya wafugaji wakianza kufurukuta kutetea haki za wafugaji , hili wanalifanya japo wakijua kwamba serikali ya CCm haina sera ya wafugaji japo ina sera ya mifugo.

Hiki ni kiini macho kwa taifa kuwa na sera ya mifugo bila kuwa na sera ya kuendeleza wafugaji.Hakuna kikundi cha Watanzania kilichozalaulika na kunyimwa haki za kibinadamu kama wafugaji.

Kwanza walinyang’anywa ardhi yao ya kufugia ,nyumba zao kuchomwa moto katika wilaya ya Hanang’.Huko serikali ilianzisha mashamba makubwa ya kilimo cha nga’no.

Wafugaji wale hawakupata fidia wala ardhi mbadala na sasa wamesambaa kila mahala nchini Mvomero , Ihefu na kwingineko.Kama vile hiyo haitoshi mahakama za nchi hazikuwasaidia wafugaji hao walipo kwenda kudai haki zao mahakamani.

Hii inaonekana kwamba kwa ujumla wake sera na sheria za nchi kwa ujumla wake zinalinda na kutetea wakuliwa na haziwalindi wafugaji.

Kule Mkomazi, wafugaji waliokuwa wakiongozwa na Lakei Faru Parutu walifukuzwa ndani ya hifadhi na bila fidia wala ardhi mbadala.Leo hii wanatangatanga bila kujua wapi walishie mifugo yao.

Lakini tumemsikia Mbunge wao Anna Kilango akiwatetea na kutaka watafutiwe maeneo mbadala ya kulisha mifugo yao na wejengewe huduma za kijamii ili jamii yao iweze kujisikia kuwa ni binadamu kama wengine.

Tukizungumiza suala zima la maendeleo , Wakulima maskini wa nchi hii ambao ndiyo waliowengi kuliko kundi lolote nchini,wamesahauliwa, kule vijijini hatuoni miradi ya umwagiliaji maji ikizinduliwa wala hatuoni wagani wa kilimo ambao wangewaongoza na kuwashauri wakulima kuhusu kilimo bora na cha kisasa.

Ama kwa hakika kila aliyewahi kutembelea vijijini siku za hivi karibuni atakuwa ameshuhudia jinsi jembe la mkono linavyowadidimiza wakulima wetu na kuwakatisha tama.

Kilimo cha kutumia jembe bila pembejeo na kutegemea mvua kimewaweka wakulima katika maisha magumu na wala wimbo huu wa maisha bora hauna maana kwao.

Tungetamani kama wakulima kwa umoja wao wangetambua hilo na kuwanyima kura hawa viongozi matapeli wa kisiasa wanaojipitisha pitisha sasa na kuwalambalamba miguu huku wakiwamwagia sifa na zawadi lukuki.

Ni vyema wakulima wajue kwamba hakuna kiongozi atakaye wakomboa kutokana na hali ngumu ya maisha inayowakabili ila wao wenyewe.

Watambue pia kwamba kila wanapopokea rushwa inayoletwa kwa sura ya ukarimu wanapunguza uhuru wao kwa kujitia minyororo na kujilaani wenyewe na kubaki maskini wenyewe.

Kwa upande wa Wafanyakazi, kipindi cha serikali ya awamu ya nne kimekamilisha mzunguko wa gurudumu la Utandawazi kwa maana kwamba uporaji wa rasilimali za viwanda na migodi sasa umetimia kwa kuwa sekta hizo zimetekwa na wageni.

Pamoja na hilo licha wafanyakazi wengi kustaafishwa kwa masurufu ‘kiduchu’, sekta ya ajira sasa inaendelea kutegemea wataalamu wageni kuliko wataalamu wenyeji.

Na hiyo sasa kwa kadri itakavyokuwa tabaka la wafanyakazi litaendelea kufifia kipato chake kitaendelea kuwa kidogo kwakuwa serikali imeshindwa kuwa na sera inayoboresha taaluma ya kazi na sera inayoboresha uongozi wa Vyama vya Wafanyakazi.

Vyama vya Wafanyakazi vipo kama havipo au kwa lugha nyingine ‘vipo vipo tu’.Kule migodini zipo taarifa za unyanyasaji kwa wachimbaji na mainjiinia wazawa na tunajua kwamba nafasi nyeti kwenye maeneo ya madini yanapokusanywa ili kupakiwa na kusafirishwa zipo mikono mwa wageni na hakuna mwenyeji anayeruhusiwa kuzisogelea.

Tunajua vile vile wenyeji hawana ushiriki wowote katika uuzaji na usafirishaji wa madini na kwamba takwimu za madini ni uongo na wizi mtupu.

Basi ni vyema wakati tukijadili hoja za kuwadia kwa uchaguzi wa Serikali za Mtaa mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani,tuangalie pia nafasi ya vyombo vya habari.

Katika uchaguzi mkuu uliopita , vyombo vya habari viliwashawishi wananchi kuchagua viongozi wa awamu ya nne.Vilifanya hivyo kwa ushawishi mkubwa na kila kalamu na ulimi ulitumika kumsifia Jemedali wa awamu ya nne, Kikwete, alivyobora, alivyo ‘Hand Some boy’ ,alivyo kijana, anavyopendwa na anavyotufaa kutuongoza.

Hata ikafikia pahala baadhi ya viongozi wa dini wakaitimisha kwa kusema hilo ni chaguo la mungu. Sasa tujiulize kama vyombo hivi vya habari viliwatendea Watanzania haki?

Hayo maisha bora kwa kila mtanzania yako wapi?Mbona vyombo hivi hivi vya habari haviulizi maswali magumu kujua kama wizi unaotokea sasa ndiyo yale maisha bora tuliyoaidiwa?

Lakini hivi sasa kwa namna moja au nyingine tumegundua baadhi ya vyombo na waandishi wa habari tayari wameishaweka sawa kuanzisha kampeni ya kuirejesha serikali ya awamu ya nne madarakani.

Sasa tujiulize hilo wanalifanya kwa maslahi ya nani?Ni vyema tuayeseme haya sasa kwani taaluma ya uandishi wa habari ipo matatani,tukifanya yale baadhi yetu waliyofanya mwaka 2005,taaluma hii itakufa.

Tutaonekana ni wahuni, wazandiki na wabababishaji malaya.Kama ni njaa basi njaa yetu aiwezi kumalizwa kwa hivyo vijisumni tunavyopewa na wanasiasa kama mbwa koko.

Ni afadhali tukajiheshimu na kuheshimu taaluma yetu hata kama itatulazimu kufa njaa.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 18 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.