Header Ads

MFANYABIASHARA MWINGINE KORTINI KWA WIZI WA MABILIONI BENKI

*Ahusishwa na wizi wa Barclays

Na Happiness Katabazi

MFANYABIASHARA maarufu wa madini nchini, Justice Deodatus Rugaibula (36), mkazi wa Msasani Beach, Alhamisi iliyopita alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na kesi ya wizi wa dola za Kimarekani milioni 1.08, (sawa na sh bilioni 1.4) kwa njia ya mtandao wa kompyuta, mali ya Benki ya Barclays.

Rugaibula ambaye hivi sasa jina lake limekuwa likitajwatajwa kwenye baadhi ya nyimbo za bendi maarufu za muziki wa dansi nchini ikiwemo bendi ya FM Academia ‘Wazee wa Ngwasuma’, alifikishwa mbele ya Hakimu Eva Nkya na ilidaiwa na wakili wa serikali kuwa anakabiliwa na mashtaka sita ya wizi kwa kutumia mtandao.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ambapo kesi hiyo ya jinai imepewa namba 75 ya mwaka huu, mashtaka hayo baadhi yake yanafanana na mashtaka yanayowakabili wafanyakazi saba wa Barclays na Mkurugenzi Mtendaji wa Dar es Salaam, Cement Muslim na mfanyabiashara maarufu wa mafuta nchini, Merey Ally Saleh (41) maarufu kwa jina la Merey Balhabou na Meneja Mwendeshaji wa Kigamboni Oil Co. Ltd, Abdallah Said Abdallah (48).

Kufikishwa kwa kumshitakiwa huyo mahakamani wiki iliyopita kumesababisha watuhumiwa wa wizi katika benki hiyo ya Barclays kufikia 10 hadi sasa.

Mwendesha mashtaka Inspekta Emma Mkonyi mbele ya Hakimu Mkazi Eva Nkya, alidai kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na mashitaka ya kula njama kwa nia ya kudanganya kwamba, Oktoba 29-30 mwaka jana, katika eneo lisilofahamika jijini Dar es Salaam, kwa kutumia ujanja, alifanya udanganyifu na kuibia benki hiyo dola za Kimarekani milioni 1,081,263.00.

Inspekta Mkonyi alidai kuwa, katika shitaka la pili, Oktoba 27 mwaka jana, katika eneo lisilofahamika jijini alighushi ujumbe wa kasi (swift message) wenye namba SEQ 000303, kuonyesha kwamba ujumbe huo ulielekea Kigamboni Oil Co. Ltd, kwenye akaunti namba 8001993 kwa ajili ya kuhamisha dola za Kimarekani 700,769.00 kinyume na sheria.

Katika shtaka la tatu, alilodai kuwa ni la kughushi, kwamba mnamo Oktoba 27, mwaka jana, Justice Rugaibula, katika eneo lisilofahamika kwa nia ya kudanganya, walighushi ujumbe wa kasi, wenye namba SEQ 00041, kuonyesha kwamba ujumbe huo unakwenda Kigamboni Oil Co. Ltd, kwenye akaunti namba 8001993 kwa ajili ya kuhamisha dola za Kimarekani 299,974.00 mali ya benki hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Inspekta Mkonyi aliendelea kudai kuwa shitaka la nne ni wizi, kwamba mshitakiwa mnamo Oktoba 31, mwaka 2002 katika Benki ya Stanbic, tawi la May Fair jijini Dar es Salaam, bila uhalali wowote katika akaunti namba 0222824801, alihamisha isivyo halali dola 200,000.00 kwenye akaunti hiyo fedha ambazo ni mali ya Benki ya Barclays (T) Ltd.

Aidha katika shitaka la tano, mshitakiwa huyo anaidaiwa kuwa Oktoba 31 mwaka 2002 katika benki ya Stansbic Tawi la May Fair jijini Dar es Salaam, bila uhalali wowote kupitia akaunti namba 012282480 aliiba fedha taslimu sh 200,000.00 kwa kutumia hundi namba 000001, mali ya Benki ya Barclays (T) Ltd.

Aidha alidai shitaka la sita ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo alidai kuwa Oktoba 31 mwaka 2008 katika Makao Makuu ya Benki ya Barclays mtaa wa Ohio jijini, baada ya kuwasilisha hati za uongo, alijipatia sh. 583,620,000 kutoka kwa Daudi wa Kigamboni Oil Co. Ltd na baada ya kupata hizo fedha alidai kuwa hayo ni malipo halali toka kwa mteja wake ambaye wamewekeza naye katika mradi wa machimbo ya madini katika mkoa wa Mara huku akijua si kweli.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshitakiwa alikana shitaka na Hakimu Nkya alisema masharti ya dhamana ni sawa na yaliyotolewa kwa washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wapo nje kwa dhamana.

Hata hivyo mshitakiwa huyo alipata dhamana.Mbali Rugaibula, wengine ni Merey na Abdallah ambao walifikishwa Machi 5, mwaka huu. Washtakiwa wengine ni ambao walifikishwa mahamani hapo mwishoni mwaka jana ni wafanyakazi wa benki hiyo ni Winford Mwang’onda, Shubira Mutungi, Naima Saria, Upendo Mushi, Magreth Longway, Emmanuel Mukoni na Ramadhani Khamis.

Mapema Machi mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, alitahadharisha mabenki kuwapo kwa mbinu mpya ya wizi unaotumia teknolojia ya kisasa ya kompyuta ambapo benki za CRDB na Barclyas zilishakumbwa na wizi huo.

Alisema aina hiyo ya wizi ni ngeni nchini na wahusika wanaweza kuchota fedha nyingi kuliko wizi uliozoeleka wa kughushi hundi, saini au ule unaofanywa kwa kuvamia na kupora kwa nguvu kutumia silaha za moto.

Alisema wizi huo umeanza kujitokeza zaidi kuanzia mwaka jana, ambapo wezi hao wa mtandao wa kompyuta walifanikiwa kuwashawishi baadhi ya wafanyakazi wa benki na watu wa kupitisha fedha hizo kwenye akaunti zao.

Wiki chache zilizopita, iliripotiwa kuwa kikundi cha watu wachache walichukua sh. bilioni 5, mali ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), kwa njia hiyo mpya ya wizi, zilizokuwa ni malipo ya kawaida kwenda Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Kwa mujibu wa taarifa hizo, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti mbalimbali ikiwamo akaunti ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ambapo ziliingizwa zaidi ya sh. milioni 671 kwenye akaunti yao iliyopo katika Benki ya CRDB, tawi la Lumumba bila wahusika kujua.

Ilielezwa kuwa fedha hizo hazikuwa za TUCTA wala chama chochote chenye uhusiano nayo, na hawajawahi kufanya biashara yoyote na TTCL kuweza kulipwa kiasi hicho cha fedha.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Machi 25 ,2009

No comments:

Powered by Blogger.