Header Ads

SERIKALI YAFUNGA USHAHIDI KESI YA MARANDA

Na Happiness Katabazi

UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), inayomkabili Mweka Hazina wa CCM MKoa wa Kigoma, Rajabu Maranda na Farijara Hussein, jana ulifunga ushahidi wake.

Wakili Kiongozi wa Serikali Stanslaus Boniface ambaye alikuwa akisaidiana na Vitalis Tomin aliliambia jopo la Mahakimu Wakazi wa Tatu, Cypriana William, Phocus Bambikya na Saul Kinemela jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, walisema wamefunga ushahidi huo shahidi wa tisa, Steven Mwakalukwa(54) ambaye ni Mkaguzi wa Mahesabu ya Ndani katika Benki Kuu kumaliza kutoa ushahidi wake.

“Waheshimiwa Mahakimu Wakazi leo (jana) ninayo furaha kubwa kuiambia mahakama hii tukufu kwamba sisi upande wa mashtaka tumefunga ushahidi wetu,” alieleza Boniface huku akionekana kuwa mwenye furaha.

Hata hivyo, Desemba mwaka jana, Boniface wakati akisoma maelezo ya awali ya kesi hiyo aliambia mahakama hiyo kuwa kesi ambayo alianza kusikiliwa mapema mwaka huu, watakuwa na mashahidi 22.

Kwa upande wa wakili wa utetezi, Majura Magafu, aliomba upande wa mashtaka uwapatie mwenendo wa kesi, ili waweze kutumia kifungu cha 230 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya 2002, ili mahakama iweze kuamua kwamba washtakiwa wana kesi ya kujibu au la.

Pia Magafu aliwasilisha aliomba wateja wake waruhusiwe kwenda nyumbani kwako Kigoma kwa mapumziko.

Akitoa uamuzi wa maombi hayo, Hakimu William alisema anakubalina na ombi la upande wa utetezi upewe mwenendo wa kesi mapema na kwamba anawaruhusu washtakiwa kwenda Kigoma ila ruhusa hiyo ni kwa ajili ya kesi hiyo na si kwenye kesi nyingine zinazowakabili washtakiwa hao.

“Ruhusa ya kwenda Kigoma imekubaliwa ila ni katika kesi hii peke yake kesi nyingine ruhusa hii isitumike tafadhali na hivyo naairisha kesi hii hadi April 15 mwaka huu, kesi hii itakuja kwa ajili ya kutajwa,” alisema William.

Washitakiwa hao wanadaiwa kula njama, kughushi, wizi, kuwasilisha hati za uongo na kujipatia ingizo la fedha kwa njia ya udanyifu kwenye akaunti , sh bilioni 1.8 mali ya BoT wakijaribu kuonyesha kampuni yao ya Kiloloma Brothers imepewa idhini ya kukusanya deni la kampuni ya BC Cars Export ya Mumbai India.

Mapema jana akiongozwa kutoa ushahidi wake na mawakili hao wa serikali Mwakalukwa aliambia mahakama mwaka 2005 akiwa Msimamizi wa Idara ya Fedha za Nje aliliona jarada la Kiloloma &Brothers ambalo lilifika katika idara yake lilokuwa likitaka lilipwe fedha za madeni na yeye pamoja na maofisa wenzake waliidhinisha kampuni hiyo ilipwe Sh 1,864,949,294.45 kupitia benki ya United Bank of Afrika.

Maranda anakabiliwa na kesi nne za aina hiyo katika mahakama hiyo wakati Farijara anakabiliwa na kesi mbili za tatu aina hiyo mahakamani hapo na wote wapo nje kwa dhamana.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumanne,Machi 24 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.