Header Ads

MTEULE WA RAIS KIKWETE ATAJWA KESI YA EPA

*Adaiwa kumuomba rushwa mtuhumiwa

Na Happiness Katabazi

MSHITAKIWA wa pili katika kesi ya wizi wa sh bilioni 1.8 za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania, Rajabu Maranda, ameiambia mahakama kwamba aliyekuwa mjumbe wa timu ya rais ya kuchunguza wizi wa fedha za akaunti hiyo, Fidelis Kairu ambaye pia ni Mkuu wa Takukuru-Kigoma, alimuomba rushwa.
Maranda alitamka hayo jana wakati alipokuwa akitoa ushahidi wake kwenye kesi ndani ya kesi ambapo alidai kuwa Kairu ndie alikuwa akimuhoji katika timu hiyo iliyokuwa na ofisi zake Mikocheni ambapo alidai kabla ya kuanza kuhojiwa alimkataa kwa sababu ana ugomvi naye.

“Waheshimiwa mahakimu, huyu Kairu nina ugomvi naye mkubwa sana kwani aliniombaga rushwa hadi akaamishwaga Kigoma, na kabla sijaanza kuhojiwa nilimkataa na wajumbe wakaniambia nisiwafundishe kazi na eti nani alinituma niibe fedha za EPA,” alidai Maranda na kusababisha watu kuangua vicheko.

Aliendelea kueleza kwamba wakati anachukuliwa maelezo ya onyo hakupewa haki zake kama kusomewa maelezo aliyochukuliwa, na wala hakuelezwa kuwa maelezo yale ni ya onyo na kwamba yangekuja kutumika mahakamani, na wala hakupewa nakala kuyasoma na kwamba alichukuliwa maelezo hayo wakati akiwa na maumivu makali na afya yake haikuwa nzuri.

“Na kwa kuthibitisha mimi nilikuwa mgonjwa, nimeleta vyeti vyangu vinavyoonyesha kwamba nilikuwa mgonjwa mahututi na nililazwa Hospitali ya Regency Upanga, na nilikuwa nikisumbuliwa na figo, na hata leo hii ninavyotoa ushahidi hapa mtukufu hakimu na mahakama yako tukufu ini langu limesinyaa,” alidai Maranda ambaye jana alionekana kuwa nadhifu baada ya kuvalia vazi la suti.

Jopo la mahakimu wakazi watatu linaloongozwa na Cypriana William, Phocus Bambikya na Saul Kinemela lilipokea vyeti hivyo vya hospitali vilivyowasilishwa na Maranda.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali, Vitalis Timon na Maranda:

Wakili: Maranda unajua kusoma na kuandika?
Maranda: Najua.
Wakili: Unakubali kwamba ulichukuliwa maelezo na SSP-Salum Kisai?
Maranda: Sikutoa maelezo bali maelezo yale nilijaziwa na SSP-Kisai.
Wakili: Ulitia saini maelezo yako?
Maranda: Nilitia saini.
Wakili: Unakubali kwamba Oktoba 7 mwaka jana, pia ulirudi Mikocheni na kuchukuliwa maelezo na Kisai?
Maranda: Nilikwenda lakini nilikwenda huku nikiwa nachechemea.
Wakili: Unakubali kwamba ulipewa kiti kizuri na Kisai?
Maranda: Wala siyo kiti kizuri.
Wakili: Ulikuwa na afya nzuri?
Maranda: Afya mbaya sana.
Wakili: Katika vyeti ulivyovitoa mahakamani leo (jana) mbona havionyeshi Oktoba 6-7 mwaka jana ambazo ndizo tarehe ulizohojiwa, kwamba ulikuwa unaumwa?
Maranda: Hata wewe wakili umewahi kuumwa, hivi ukienda leo kwa daktari anaanza kukutibia leo leo? Hivyo ni vyeti nilivyofanyiwa vipimo.
Wakili: Nakuuliza, mbona vyeti hivi havionyeshi kwamba tarehe hizo wewe ulitibiwa?
Maranda: Ni hivi, nilikwenda hospitali kutibiwa sikwenda hospitali kwa ajili ya malumbano.
Wakili: Ulianza kuugua mwaka gani?
Maranda: Novemba 2007.
Wakili: Hiyo ilikuwa ni baada ya sakata la EPA kuanza?
Maranda: Hapana.
Wakili: Maranda umewahi kuugua ugonjwa wa akili?
Maranda: Hata degedege sijawahi (watu wakaangua kicheko).
Wakili: Mei 16 mwaka jana saa nne asubuhi ulifika ofisi za Task Force, unakubali?
Maranda: Inawezekana kwani nimekwenda mara nyingi.
Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano kati ya wakili wa Serikali Michael Lweno na Maranda:
Wakili: Hoja yako ya msingi kwamba tarehe hizo ulizokuwa ukihojiwa ulikuwa mgonjwa?
Maranda: Ndiyo.
Wakili: Mbona vyeti ulivyovitoa hapa mahakamani havionyeshi tarehe hiyo?
Maranda: Kimya.
Wakili: Unakubaliana na mimi vyeti vyako havionyeshi kuwa ulishawahi kulazwa ICU na kufanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Regency?
Maranda: Kimya.
Wakili: Unakubaliana na mimi kwamba hivi vyeti havionyeshi Novemba 2007 ambapo ulidai uligundulika kuwa na matatizo ya figo?
Maranda: Kimya.
Wakili: Iambie mahakama maelezo ya kwanza uliyoyaandika kwenye Task Force wakati ukiwa na wakili, na yale uliyochukuliwa wakati haukuwa na wakili wako yanafanana?
Maranda: Ndiyo yanafanana kwa asilimia 95.
Wakili: Ni lini ulikumbuka kwamba hukupewa haki zako na timu hiyo?
Maranda: Kimya.
Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake, Hakimu Mkazi William aliahirisha kesi hiyo hadi leo ambapo watatoa uamuzi kuhusu ushahidi ulitolewa na Maranda kwenye kesi ndogo.

Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Jumatano, Februali 4 mwaka 2009

No comments:

Powered by Blogger.